Changamoto za Mifumo ya TEHAMA Katika Kukuza Uwajibikaji Nchini

Na Octavian Swai

Juni 28, 2021 WAJIBU ilizindua ripoti za uwajibikaji kwa mwaka 2021. Ripoti hizi ambazo zimekuwa zikitoka kwa mwaka wa tano sasazimerahisishwa kutoka katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambazo hutolewa kila mwaka.

Mwaka huu ripoti za Uwajibikaji zilizinduliwa na Bw. Charles Mpaka Afisa kutoka katika Ofisi ya Msajili wa AZAKI kwa niaba ya Msajili wa AZAKI Bi. Vickness Mayao terehe 28 Juni, 2021 katika ukumbi wa Kitenga, Royal Village Hotel, Dodoma. Mada kuu iliyojadiliwa katika uzinduzi huo ilikuwa ni “Changamoto za Mifumo ya TEHAMA katika kukuza Uwajibikaji Nchini” ambayo iliwasilishwa na Bi. Sultana Seif kutoka Mamlaka ya Serikali Mtamdao (eGA).

Kwa mwaku huu, WAJIBU imezindua ripoti tatu za uwajibikaji ambazo ni; Ripoti ya Uwajibikaji – Serikali Kuu na Mashirika ya Umma, Ripoti ya Uwajibikaji – Serikali za Mitaa na Miradi ya Maendeleo pamoja na Ripoti ya Uwajibikaji ya Ufanisi, Rushwa na Ubadhirifu katika Sekta ya Umma.

Katika uzinduzi huo, kulikua na uwakilishi kutoka Bungeni (Wabunge), OR-TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tume ya Maadili, Mamlaka ya Serikali Mtamdao (eGA), NIDA, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Msajili wa AZAKI, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, AZAKI pamoja na vyombo mbalimbali vya habari.

Tukio hilo la uzinduzi lilifunguliwa na Mkurungezi Mtendaji wa WAJIBU Bw. Ludovick Utouh. Katika ufunguzi huo, Bw. Utouh aliipongeza Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) kwa kuwasilisha ripoti za ukgauzi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati uliopo kisheria.

“Kwa mwaka huu CAG aliwasilisha kwa Mhe. Rais jumla ya Ripoti 21; kati ya hizo, Ripoti 15 ni za ufanisi na Ripoti 6 ni za ukaguzi wa hesabu za fedha” alisema Bw. Utouh.

Akieleza lengo la WAJIBU kuandaa ripoti za uwajibikaji, Bw. Utouh alisema kuwa, wananchi wengi wamekua wakipata changamoto katika kuzielewa ripoti za CAG kutokana na ugumu wa lugha za kitaalam zinazotumika na pia ukubwa wa ripoti husika. Vilevile, CAG amekua akitoa mapendekezo mengi kwenye ripoti zake lakini hakujawa na msukumo wa umma juu ya utekelezaji wa mapendekezo hayo. Hivyo basi, changamoto hizo ndizo zilipelekea WAJIBU kuandaa ripoti hizi za uwajibikaji.

“Ripoto zinazozinduliwa ni ripoti tatu ambazo ni; Ripoti ya uwajibikaji Serikali Kuu na Mashirika ya Umma, Ripoti ya uwajibikaji Mamlaka ya serikali za Mitaa na Miradi ya Maendeleo na Ripoti ya tatu ni ripoti ya Ufanisi, Rushwa na Ubadhirifu Katika Sekta ya Umma ya mwaka 2021” alisema Utouh.

Katika uzinduzi huo kuliwa na mawasilisho mawili yaliyofanywa na Meneja wa miradi kutoka WAJIBU Bw. Moses Kimaro pamoja na Bi. Sultana Seif kutoka Mamlaka ya Serikali Mtamdao (eGA).

i. Wasilisho la Uchambuzi wa Ripoti za CAG Mwaka 2019/20 – Ripoti ya Ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA

Bw. Moses Kimaro akitoa wasilisho lake katika uzinduzi wa Ripoti za Uwajibikaji Juni 28, 2021 katika Hotel ya Royal Village DODOMA

Wasilisho hili lillilojikita kwenye mada kuu ya uzinduzi, ilitolewa na Meneja wa Miradi – WAJIBU Bw. Moses Kimaro. Katika wasilisho hilo, alionesha namna mifumo ya TEHAMA inavyoathiri uwajibikaji nchini. Aliezeza changamoto mbalimbali zinazoikumba mifumo ya TEHAMA Serikalini. Changamoto zilizobainishwa ni kama zifuatazo;

 1. Miongozo ya usimaizi wa mitandao serikalini (guidelines) kutozingatiwa
 2. Ukosefu wa umiliki wa mifumo ya TEHAMA, (licencing)
 3. Utunzaji duni wa Seva na KanziData, (Server & database safety)
 4. Uwezo mdogo wa mifumo katika kuendesha shughuli za serikali (automation/system’s procedures)
 5. Uendeshaji duni wa mifumo katika kusimamia bajeti ya serikali, (systems controls/authorization levels)
 6. Mifumo miwili kutumika kufanya kazi zinazofanana (ovelapping)
 7. Gharama kubwa za uendeshaji wa mifumo (maintance costs)
 8. Ukosefu wa Mafunzo ya kuuelewa na kuutumia mfumo (training)
 9. Kazi kufanyika nje ya mfumo (bypassing/Manual)
 10. Mifumo kutofanya kwa muingiliano (linking/integration)
 11. Masuala ya kiusalama katika mifumo (systems security)

Kwa mujibu wa Bw. Kimaro, changamoto hizi kwa kiasi kikubwa zimezorotesha ufanisi wa mifumo hii kwa kiasi kikubwa sana. Mbli na kuzorotesha ufanisi, pia zimeongeza garama za uendeshaji ya mifumo husika.

Baada ya wasilisho hilo, ripoti tatu za uwajibikaji kwa mwaka 2019/20 zilizinduliwa rasmi na Bw. Charles Mpaka kwa niaba ya Msajili wa Hazina Bi. Vicknes Mayao.

Mwakilishi wa Msajili wa AZAKI Bw. Charles Mpaka akikata utepe kuzindua ripoti za Uwajibikaji za mwaka 2019/20

ii. Wasilisho la “changamoto za mifumo ya tehama katika kukuza uwajibikaji serikalini”

Wasilisho hili lilifanywa na Bi. Sultana Seif kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA). Katika wasilisho lake, Bi. Sultana aliongelea changamoto zilizopo katika utekelezaji wa serikali mtandao. Changamoto hizo ni;

 1. Uwepo wa Mifumo mingi tumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma isiyoweza kubadilishana taarifa,
 2. Uwepo wa Mifumo ambayo haijumuishi taratibu za utendaji kazi kuanzia mwanzo hadi mwisho (end-to-end business processes) katika baadhi ya taasisi za umma, hivyo kusababisha taratibu zingine kufanyika nje ya mfumo au kwa kutumia mifumo mingine isiyowasiliana,
 3. Kuendelea kuwepo kwa utegemezi mkubwa wa wakandarasi (vendors) katika Kusanifu, Kujenga na Kuendesha Mifumo mhimili (Critical Systems),
 4. Upungufu wa watumishi wenye uadilifu, ujuzi na weledi, pamoja na mafunzo maalum ya ubobezi (specialized trainings) yanayotakiwa katika Usanifu, Ujenzi na Uendeshaji wa Mifumo na Miundombinu na Usalama wa TEHAMA katika Taasisi za Umma,
 5. Baadhi ya mifumo inayotoa huduma kuhifadhiwa katika mazingira duni na yasiyo salama, hivyo kutofanya kazi kwa ufanisi tarajiwa pamoja na kuhatarisha usalama wa taarifa zilizomo
 6. Kukosekana kwa vituo au vifaa mbadala vya kujikinga na majanga, hivyo kusababisha huduma kutokuwa za uhakika hasa inapotokea hitilafu kwenye mifumo au miundombinu ya msingi ya Serikali mtandao,
 7. Kutozingatiwa kikamilifu kwa viwango na miongozo ya usalama katika kutekeleza baadhi ya mifumo na miundombinu ya TEHAMA, ikiwa ni Pamoja na kutofanyiwa ukaguzi wa kiusalama, hali inayopunguza ufanisi na kuhatarisha usalama wa taarifa za Serikali,
 8. Udhibiti mdogo wa matumizi ya mifumo ya TEHAMA, na
 9. Udhaifu katika kushughulikia vihatarishi vya matishio ya kiusalama mtandaoni.

Bi. Sultana Seif akitoa wasilisho lake katika uzinduzi wa Ripoti za Uwajibikaji Juni 28, 2021 katika Hotel ya Royal Village DODOMA

Mbali na uwepo wa changamoto hizi, Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) imechukua hatua mbalimbali ili kutatua changamoto hizo. Kwanza, Serikali imeanza na jitihada za kutengeneza mfumo wa kubadilishana taarifa (Government Enterprise Service Bus) kwa ajili ya kuwezesha Mifumo tumizi ya taasisi za Umma kubadilishana taarifa kwa urahisi, Kuendelea kwa shughuli za mapitio na tathmini za Usalama wa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA, Kuendelea kutoa ushauri wa kitaalam na msaada wa kiufundi katika shughuli za Utengenezaji, Usimamizi na Uendeshaji wa Mifumo na Miundombinu ya TEHAMA ya Serikali ili kuhakikisha inazingatia sheria, kanuni, taratibu, viwango na miongozo iliyoidhinishwa. Vilevile, kuendelea kuimarisha uwezo wa kujikinga na uhalifu wa mtandaoni kabla ya kuleta madhara kwenye Mifumo na Miundombinu ya Serikali, Kuendelea kutoa mafunzo ya kitaalamu na ya ubobezi ya muda mfupi na muda mrefu kwa watumishi wa TEHAMA kwa ajili ya kuongeza ujuzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea kwa kasi kubwa duniani pamoja na kuanza kutekeleza mapendekezo ya CAG kuhusiana na mapungufu yaliyobainika katika mifumo ya TEHAMA ya Serikali.

Wabunge wakiwa katika uzinduzi wa Ripoti za Uwajibikaji Juni 28, 2021 katika Hotel ya Royal Village DODOMA

Baada ya mawasilisho hilo mawili, washiriki walipewa fursa ya kujadilikwa pamoja. Asilimia kubwa ya wachangiaji walijitika katika kuishauri serikali kuunganisha mifumo ya utendaji inayoonekana inafanya kazi zinazofanana. Vilevile, Taassi za serikali zilisisitizwa kufuata Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019. Pia, eGA walishauriwa kutoa elimu kwa umma juu ya hiyo taasisi na majukumu yake maana inaonekana wananchi wengi hawaijui.

Baadhi ya Wabunge waliohudhuria katika uzinduzi huo walishauri eGA kuhakikisha kuwa mifumo yote ya serikali inamilikiwa na taasisi husika ili kuepuka changamotot za uendeshaji ikiwemo utunzaji wa taarifa. Pia, walishauri katika hii mifumo ya serikali kuwe na “backups” ya mifumo ili inapocheza/kupata tatizo hiyo backup isaidie kutoa huduma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Neghenjwa Kaboyoka (Mb) pamoja na mambo mengine, aliishauri WAJIBU kuandaa warsha ya pamoja na eGA pamoja na wabunge kwa lengo la kujadili kwa pamoja namna ya kuunganisha hii mifumo ya serikali kwa lengo la kuleta ufanisi katika utendaji.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Japhet Hasunga akiongea katika uzinduzi wa Ripoti za Uwajibikaji Juni 28, 2021 katika Hotel ya Royal Village DODOMA

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati hiyo ya PAC ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Vwawa Mhe. Japhet Hasunga alishauri ili kuwepo na mifumo inayoendana ni vyema watendaji (wataalamu) wa serikali wafanye kazi kwa ukaribu na wanasiasa.

Lengo la ukaribu huo ni kurahisisha utendaji pale wanapokumbana na changamoto au kuleta ubunifu wa mfumo mwanasiasa atarahisisha kulipekela mbele zaidi kwa ajili ya majadiliano. Pia alishauri serikali iwekeze kwenye rasilimali watu ili kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye mifumo ya serikali. Katika kuhitimisha, Mhe. Hasunga aliiomba WAJIBU kuandaa mafunzo ya namna ya kufanya uchambuzi wa ripoti za ufanisi kwa wabunge kwani kwao imekua changamoto kidogo kuzielewa ripoti hizo.

Mwishoni mwa tukio la uzinduzi, yalitolewa mapendekezo ya kutekeleza kwa upande wa WAJIBU na upande wa Serikali kupitia Wakala wa Serikali Mtandao (eGA). Mapendekezo hayo ni;

 1. WAJIBU iandae warsha ya kuwajengea uwezo wabunge husuan kamati za usimamizi za Bunge za PAC, LAAC, PIC pamoja na kamati ya Bunge ya bajeti juu ya uchambuzi wa ripoti za ukaguzi wa ufanisi zinazotolewa na CAG,
 2. WAJIBU kuandaa warsha ya kuwaleta pamoja Wakala wa Serikali Mtandao eGA pamoja na kamati za Bunge za usimamizi na kujadili changamoto za mifumo hii ya TEHAMA na namna ya kutatua changamoto hizo.
 3. Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) iangalie namna ya kutoa elimu kwa umma juu mifumo hii ya TEHAMA na matumizi yake serikalini.

Tukio la uzinduzi wa ripoti za uwajibikaji lilifungwa na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Foundation for Civil Society (FCS) Bw. Francis Kiwanga. Katika kuhitimisha uzinduzi huo, Bw. Kiwanga aliwashukuru washiriki kwa kufika pamoja na kujadili kwa pamoja changamoto zinazoikabili mifumo ya TEHAMA ya serikali. Alisisitiza kutekeleza mapendekezo/maazimio yaliyoyolewa.