Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Mstaafu) ambae kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU – Institute of Public Accountability Bw. Ludovick Utouh ametaja athari zinazoweza kujitokeza ikiwa Serikali itashindwa kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na CAG.
Akizungumza Agosti 3, 2020 Jijini Dodoma katika uzinduzi wa ripoti za uwajibikaji zilizoandaliwa na taasisi ya WAJIBU, Bw. Utouh alisema kutoteelezwa kwa mapendekezo hayo kunaweza kuisababishia Serikali kukusanya mapato kidogo kuliko yaliyokusudiwa.
Ripoti hizi za uwajibikaji ni ripoti ambazo zinarahisishwa kutoka kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Ripoti hizi WAJIBU huzitoa kila mwaka mara tu CAG anapotoa ripoti zake za ukaguzi.
Lengo kuu la ripoti hizi ni kuhimiza utekelezwaji wa mapendekezo yanayotolewa na CAG katika ripoti zake za ukaguzi.
Katika uzinduzi wa ripoti hizo za uwajibikaji Bw. Utouh alisema kuwa kutokutekelezwa kwa mapendekezo hayo ya CAG mara nyingi kunapekelea matumizi yasiyo na tija ikiwemo matumizi yasiyolingana na thamani ya fedha iliyotumika.
Bw. Utouh alitoa mfano wa Shirika la Pride ambalo hadi sasa haijafahamika mmiliki wake halali licha ya kuripotiwa kwenye ripoti za CAG tangu mwaka 2012.
“Kwa Serikali kutokushughulikia hili la Pride tangu lilivyoibuliwa mwaka 2012 hadi sasa kumesababisha taasisi hiyo kushindwa kuendelea kutoa huduma na kuwaacha watumishi wake wengi katika sintofahamu huku ikiwa na madeni lukuki. Kama hili lingeshughulikiwa mapema, hasara zinazoonekana kwa sasa zisingetokea” alisema Bw. Utouh.
Aidha alishauri kuwepo kwa mifumo thabiti ya kiuwajibikaji itakayohakikisha kuwa mapendekezo ya CAG yanatekelezwa na pale ambapo hayatekelezwi pawe na ripoti maalumu inayoeleza sababu za kutokutekelezwa kwake.
Kwa upande wake Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi Bw. Salhina Mkumba alisema kuwa kinachosababisha taasisi nyingi za umma kutofuata sheria katika usimamizi wa mali za umma ni kukosekana kwa uwajibikaji pamoja na mifumo ya udhibiti ya ndani.
“Kuna umuhimu wa kutekeleza yanayoshauriwa na CAG ili kuhakikisha kuwa malengo haya endelevu yanafikiwa kama inavyotarajiwa.
Bw. Mkumba alimuwakilisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Charles Kichere katika uzinduzi huo wa ripoti za uwajibikaji.